Thursday 28 April 2011

MESHEHA, MADIWANI PEMBA WATAKIWA KUSHIRIKIANA.

Masheha, Madiwani Pemba watakiwa kushirikiana

Na Bakari Mussa, Pemba
MASHEHA na Madiwani kisiwani Pemba, wametakiwa kufanya kazi pamoja na kujenga ushirikiano ili kupeleka mbele maendeleo ya wananchi chini ya Serikali ya Awamu ya Saba ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo katika mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Akizungumza na viongozi hao wa wilaya ya Mkoani, katika ufunguzi wa mafunzo ya uongozi juu ya Mfumo wa Serikali hiyo kwa Viongozi, katika ukumbi wa Umoja ni Nguvu Mkoani, Afisa Mdhamini Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Pemba, Jokha Khamis Makame, alisema Wazanzibari hawana budi kuufuata mfumo huo kwa vile wameukubali wao wenyewe kwa kuelewa kuwa utakuwa na maslahi kwao.
Alisema viongozi hao hawana budi kuwaelimisha dhana nzima ya utawala bora pamoja na utawala wa sheria, kwani huo ni chachu ya maendeleo jambo ambalo Zanzibar imepiga hatua kubwa na sasa amani na utulivu imeendelea kudumishwa.
Afisa huyo, alieleza pamoja na changamoto zinazowakabili viongozi hao lakini Serikali imo mbioni kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria zake kama vile Sheria No. 1/1998 na Sheria N. 3 na 4 ya mwaka 1995, ili ziandane na wakati wa sasa ziweze kufanya kazi ipasavyo kutokana na mfumo huo.
Nae Afisa Tawala wa Wilaya hiyo , Abdalla Salim Abdalla, aliishukuru Afisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kutoa mafunzo hayo kwa viongozi hao ambao wako karibu sana na wananchi ambao ndio wadau wakubwa wa maendeleo kwa nafasi walizonazo.
Alisema maelezo yaliotolewa na Afisa Mdhamini huyo, ameahidi kuyafanyia kazi katika wilaya yake kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wa wilaya hiyo, hatua kwa hatua kwa kujenga mashirikiano ya pamoja kwa lengo la kuijenga nchi yao.
Alifahamisha kuwa changamoto zilijitokeza hapo nyuma tayari zimeanza kufanyiwa kazi na sasa hivi pande zote zinashirikiana katika masuala ya kijamii na ya kiserikali bila ya kujali itikadi zao.
Aidha Mkurugenzi wa TAMISEMI Zanzibar, Naimu Ramadhani Pandu, aliwataka viongozi hao kuona haja ya ule muda walioupoteza wa malumbano ya kisiasa ambao ulidumaza kwa kiasi fulani harakati za maendeleo sasa wanaufanyia kazi kwa kujenga umoja wa Wazanzibari lengo likiwa kuleta maendeleo kwa pamoja.
Alieleza kuwa mfumo huu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa umekuwa na mabadiliko makubwa juu ya suala zima la amani ya nchi na sasa hivi hakuna anaeweza kubisha juu ya suala hilo hasa pale baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.
Hivyo aliwasisitiza kujenga mashirikiano ya pamoja na upendo bila ya kuangalia tafauti zao za itikadi za kisiasa kwa kuelewa wote ni kitu kimoja ni Wazanzibari ambao wanapaswa kuijenga nchi yao.

No comments:

Post a Comment