Saturday 30 April 2011

ZIARA DK. SHEIN YAZIDISHA USHIRIKIANO UTURUKI, ZANZIBAR.

Ziara Dk. Shein yazidisha ushirikiano Uturuki, Z’bar

Yaahidi kutuma timu ya watalaamu
‘Turkish Airline’ kutua visiwani
Na Rajab Mkasaba
RAIS wa Uturuki, Abdullah Gul amesema ziara ya rais wa Zanzibar na Mwewnyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein nchini Uturuki, ni muhimu na itazidisha ushirikiano wa kihistoria baina ya nchi hizo.
Rais Gul, alieleza hayo alipokuwa na mazungumzo na rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein katika makazi yake huko mjini Ankra.
Alisema ziara ya Dk. Shein nchini humo ni muhimu sana na itaendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo hasa kwenye nyanja ya maendeleo.
Rais Gul alisema ushirikiano kwenye nyanja za maendeleo baina ya mataifa unahitajika hivi sasa kuliko wakati mwengine wowote kutokana na ushindani wa kiuchumi uliopo.
Alisema Uturuki ina uzoefu mkubwa katika biasahara ya Utalii, hivyo Zanzabar kwa kiasi kikubwa ambayo uchuimi wake umekuwa ukitegemea utalii, itafaidika kwa kubadilishana uzoefu kwenye sekta hiyo.
Rais Gul alifahamisha kuwa upo uwezekano wa shirika la ndege la nchi hiyo, ‘Turkish Airline’, kuleta ndege zake moja kwa moja visiwani, ikiwa ni hatua moja ya kuimarisha sekta ya utalii.
Aidha nchi hiyo imeahidi kukisaidia kwa kukiongezea uwezo Chuo Cha Maendeleo ya Utalii kilichopo Maruhubi pamoja na ujenzi wa hoteli za kisasa na kushirikiana katika masuala mazima ya utamaduni.
Aidha rais Gul, aliahidi kuwa serikali yake itatuma timu ya wataalamu visiwani hapa kwa lengo la kuja kufanya tathmini ya mahitaji ya ndani ya sekta za kimaendeleo na kiuchumi ambazo inaweza kuisaidia Zanzibar.
Kwa upande wa sekta ya elimu, Rais huyo alisema kuwa Serikali ya Uturuki itashirikana na Serikali ya Mapinduzi Zanzbar katika kuimarisha sekta ya elimu hasa elimu ya juu kwa kuongeza nafasi za masomo zinazotolewa na Serikali ya Uturuki na pia, kubadilishana wataalamu baina ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na vyuo vyengie vya elimu ya juu nchini Uturuki.
Pamoja na hayo, Rais alisema kuwa Uturuki imo katika mipango ya kujenga Chuo Kikuu nchini Tanzania ambacho kitajengwa Tanzania Bara ambapo alisema kuwa Zanzibar nayo itanufaika moja kwa moja na chuo hicho.
Kwa upande wake Dk. Shein alisema kuwa wananchi wa Zanzibar wana matumaini makubwa na serikali yao na hatua za serikali ya Uturuki kuendeleza ushirikiano na Zanzibar nako kutachangia juhudi za kuendeleza na kufikia matarajio ya wananchi hao.
Aidha, Dk. Shei alisema kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar inafanya juhudi za kuimarisha sekta ya utalii na kutokana na Uturuki kupiga hatua katika seta hiyo itakuwa endapo nchi zitashirikiana pamoja.
Dk. Shein alisema kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar imefanya juhudi kubwa katika kuimarisha sekta ya elimu hasa elimu ya msingi lakini jitihada za ziada zinahitajika katika kuimarisha elimu ya juu.
Mapema Dk. Shein alifika eneo la kumbukumbu ya kiongozi wa kwanza wa nchi hiyo marehemu Kemal Atyaturk mjini Ankara na kuweka shada la maua akiwa amefuatana na mkewe Mama Mwanawmema Shein.
Baada ya hapo alikutana na Spika wa nchi hiyo katika ofisi za Bunge la nchi hiyo na kufanya mazungumzo ambayo yalilenga kuendeleza ushirikiano baina ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na Bunge la Uturuki.

No comments:

Post a Comment