Friday, 29 April 2011

MJASIRIAMALI AZOA KITITA CHA COCA COLA

Mjasiriamali azoa kitita cha Coca Cola

Na Mwanajuma Abdi
KAMPUNI ya vinywaji baridi 'Zanzibar Bottlers Ltd', imekabidhi zawadi ya fedha kwa washindi wa promosheni ya kamata kitita na Coca Cola.
Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika jana katika kiwanda cha Coca Cola huko Muembemakumbi, ambapo Meneja Uzalishaji wa kampuni hiyo Ally Kassim alimkabidhi Jabir Amour Dadi shilingi 1,000,000 baada ya kushinda kutokana na kunywa soda za kampuni hiyo.
Aidha Meneja Ufundi wa kampuni hiyo Amour Ally, aliwakabidhi washindi wawili wa shilingi laki tano kila mmoja, ambao ni Makame Juma Makame na Rajab Ibrahim Khamis.
Akizungumza mara baada ya makabidhiano hayo, Meneja Mauzo Haji Khatib, alisema promosheni ya kamata kitita na Coca Cola inaendelea hadi kesho Aprili 30, ambapo zawadi zitaendelea kutolewa hadi Mei 15.
Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kunywa soda za Coca Cola, Sprite na Fanta, ili waweze kujishindia fedha, akisema zawadi zipo nyingi zikiwemo shilingi 100,000, 50,000, 10,000, na 1,000 pamoja na soda za bure.
Akielezea furaha yake, Jabir Amour mkaazi wa Darajabovu aliyeshinda shilingi milioni moja, alisema fedha hizo zitamsaidia kuongeza mtaji wa biashara zake ndogondogo alizojiajiri.
Nae mshindi wa shilingi laki tano Makame Juma Makame, alisema baada ya kunywa soda kumi na kufanikiwa kushinda zawadi hiyo, atajiimarisa zaidi katika biashara yake ya samaki hapo Malindi.
Promosheni ya kamata kitita na Coca Cola ilianza katikati ya mwezi wa Machi mwaka huu..

No comments:

Post a Comment