Friday, 8 April 2011

LOWASA AWAANGUKIA WAMASAI WAIKUBALI SHERIA YA UFUGAJI.

Lowasa awaangukia Wamasai waikubali sheria ya ufugaji



Na Nalengo Daniel, Morogoro

MBUNGE wa Monduli ambaye pia ni kiongozi mkuu wa kabila la wamasai Tanzania na Kenya (Ole Laigwenani), Edward Ngoyayi Lowasa, amewataka wafugaji kukubaliana na sheria ya mifugo, ili kuendana na mabadiliko ya kisasa ya ufugaji.

Hayo aliyasema jana kwenye mkutano wa wakuu wa kabila la wamasai (legweinani) kutoka maeneo ya Pwani, Arusha, Morogoro, Tanga na Bagaboyo mkutano uliofanyyika katika kijiji cha Wami Dakawa Wilaya ya Mvomero mkoani hapa.

Aliwataka wafugaji hao kuzisoma vizuri sheria hizo na kutoa mapendekezo yao sehemu ambazo wanaona zinawabana ili ziweze kufanyiwa marekebisho na kwamba katika sheria hiyo baadhi ya vipengele, vinatakiwa kufanyiwa marekebisho.

Mbunge huyo wa Monduli alisema sheria hiyo ni nzuri na kwamba inasaidia kujua mifugo inapochinjwa imetoka eneo gani na kama inatokea nyama hiyo ina ugonjwa ni rahisi kuelewa eneo ilikotoka mifugo hiyo.

Lowasa aliongeza kuwa ili kuingia kwenye soko la ushindani ni muhimu wafugaji kufuga kisasa na kwamba mfugaji hawezi kuingia kwenye ushindani wa soko hilo ikiwa mifugo yake haijafugwa kisasa, na kuwataka kufuga mifugo ya unenepeshaji kibiashara ambapo watanufaika kwa kuuza ng’ombe kwa bei ya juu na kuwasaidia kuinuka kiuchumi.

Lowasa aliwataka kuingia kwenye ufugaji wa kisasa ili kuondokana na ufugaji wa kuhamahama na usio na tija kwao na kwamba hawawezi kupata maendeleo ikiwa wataendelea kuhamahama kwa kuwa ardhi inapungua.

Vile vile amewataka kuacha tabia ya kuweka alama zitakazoathiri ama kupoteza ubora na thamani ya ngozi ya Ng’ombe na badala yake amewataka waweke alama kwenye sikio.



Kwa upande mwingine Lowasa alizungumzia suala la elimu ambapo aliwashauri wafugaji hao kujenga shule za bweni badala ya za kutwa ili waweze kuwapeleka watoto wao kwenye shule hizo.

Pia alisema hatua za kisheria zitachukulia kwa mfugaji yeyote atakayeshindwa kumpeleka mtoto wake shule na kuamua kumuozesha akiwa na umri mdogo.

Mapema kwenye kikao hicho mkuu wa Wilaya ya hiyo Fatuma Mwasa aliwaomba wanawake wakifugaji kutoa taarifa kwake za kuozeshwa kwa mtoto wakike badala ya kupelekwa shule.

No comments:

Post a Comment