Monday 25 April 2011

ZANZIBAR DCMA KUWASHA MOTO UFARANSA

 Zanzibar DCMA kuwasha moto Ufaransa

Na Aboud Mahmoud


WALIMU watano wa Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi Zanzibar (DCMA), wanatarajiwa kuondoka leo kwenda Ufaransa kwa ajili ya kushiriki tamasha la muziki lijulikanalo kwa jina la 'Festival Bombard'.
Adel Dabo na Mohammed Issa Matona ambao ni miongoni mwa walimu hao wanaounda kikundi cha 'Saffar', wameliambia gazeti hili kuwa, wakiwa huko watafanya maonesho katika miji tafauti.
Waliwataja walimu wengine wataokuwa pamoja nao katika ziara hiyo, Rajab Suleiman, Godfrey Chinga na Juma Begu.
Walisema wakiwa nchini humo, watapika kambi kwenye mji wa Cleguerek na kufanya maonesho katika miji ya Pontivy na Rennes Kirgis ambapo wakijumuika pamoja na wasanii wa nchi nyengine .
"Maonesho tutakayofanya Ufaransa, yatakuwa kwa ushirikiano na wenzetu wa kutoka nchi mbalimbali ambao pia wanatumia ala ya zumari kama sisi", alisema Dabo.
Baada ya kumalizika kwa maonesho hayo ya pamoja, Dabo alisema pia wamepata mualiko maalumu wa kuonesha utamaduni wa Zanzibar, katika onesho watakalofanya peke yao.
Matona alifahamisha kuwa, heshima hiyo ya pekee waliyopewa inatokana na hamu ya watu wa nchi nyengine kutaka kujua ngoma za utamaduni wa Zanzibar, hivyo wameipokea kwa mikono miwili na kuongeza kwamba hiyo ni fahari kwa visiwa hivi.
"Kila nchi imepewa nafasi ya kufanya onesho moja katika kila mji, lakini sisi tumepewa nafasi maalumu ikikumbukwa kuwa tulipokuwa huko mwaka 2009, tuliwavutia wengi kwa jinsi tulivyofanya vyema, na Wafaransa wengi wameomba twende tena mwaka huu", alifafanua.
Ziara ya kikundi hicho cha Saffar kinachoundwa na wakufunzi wa muziki na ala za asili, inatarajiwa kuchukua muda wa wiki mbili.

No comments:

Post a Comment