Tuesday 12 April 2011

MIKOKO 21,000 KUPANDWA BUMBWINI.

Mikoko 21,000 kupandwa Bumbwini

Na Mwantanga Ame

WIZARA ya Kilimo na Maliasili inatarajia kupanda hekta sita za miti aina ya mikoko na mikandaa katika eneo la Bumbwini Mafufuni wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja.

Wizara hiyo imeamua kuchukua hatua hiyo ikiwa ni siku ya kuadhimisha siku ya upandaji miti kitaifa ambapo miti 21,000 inatarajiwa kupandwa ambapo kazi hiyo itafanyika Aprili 26, 2011.

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari Waziri wa Wizara hiyo Mansoor Yussuf Himid, alisema wameamua kulitumia eneo hilo kupanda miti hiyo ikiwa ni hatua ya kuweka mazingira bora kutokana na kuendelea tatizo la ukataji miti ovyo.

Alisema tatizo la uharibifu wa mazingira hivi sasa limekuwa kubwa duniani jambo ambalo limekuwa likisababisha kutokea kwa majanga ambayo huiathiri jamii, viumbe vya baharini, ndege na wanyama.

Kiasi cha miti ambayo hukatwa kwa Zanzibar alisema kuwa ni hekta 6,000 huku miti inayopandwa ni hekta 450 ikiwa ni sawa na asilimia 50 kiasi ambacho ni kidogo.
Alisema kuwapo kwa kiwango hicho kimeanza kuonesha dalili ya kuharibika kwa mazingira kwa kiasi kikubwa ambapo kumekuwa kukichangiwa na uchimbaji wa mchanga, huku miti ya mazao ya biashara ukiongezeka na ukataji ya mbao pamoja na dawa za misitu.

Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha kupungua kwa vyanzo vya maji, mazalio ya wanyama ndege na samaki huku miti ya aina mikandaa na mikoko ikiwa ni moja ya chanzo kizuri cha fedha za kigeni kutokana na watalii kupenda maeneo yenye uzalishaji wa miti hiyo.

Alisema kinachoonekana kuna baadhi ya watu bado hawataki kuelewa thamani halisi ya msitu na hali hiyo ikiongezeka upo uwezekano mkubwa wa kuwepo majanga.

Ili kunusuru hali hiyo Waziri huyo alisema serikali inazidi kutoa wito kwa kuzitaka taasisi zote zinazofanya kazi ya kutoa elimu juu ya suala la upandaji miti na utunzani mazingira kuifanya kazi hiyo ili kuviwezesha vizazi vijavyo viweze kunufaika na raslimali hizo.

“Kwa mara nyngine tena natoa wito kwa wananchi wote kuunga mkono juhudi za Wizara ya Kilimo na Maliasili katika kuongeza maeneo ya hifadhi ya misitu ya asili na kupanda kwani misitu ndio hazina yetu” alisema waziri huyo.

Alisema ni vyema kwa wananchi kutumia nishati mbadala ya ikiwemo ya gesi ambayo tayari serikali imeweza kuweka njia mbadala ya kuweza kuifikia nishati hiyo.

No comments:

Post a Comment