Mjadala katiba Bungeni njia panda
Pinda asema haujafikiriwa kuondolewa
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SERIKALI ya Tanzania imesema haiwezi kutoa msimamo wa kuondosha mjadala wa mswada wa katiba Bungeni, hadi hapo kamati ya Bunge itakapowasilisha maoni yake kupitia kwa Spika wa Bunge.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Mizengo Peter Pinda alieleza hayo jana Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu suali la papo kwa papo aliloulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzania alimuuliza Waziri Mkuu kwamba, mswada huo umezua hofu kwa taifa hili kutokana na uzito wake na kusababisha wananchi, wakiwemo wanasiasa, serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wadau mbali mbali kutaka kuondolewe Bungeni.
Pinda alisema hawezi kutoa maamuzi yeyote kwa sasa hadi hapo kamati ya Bunge itakapotoa maoni yake, kwani hata yeye ni Mtanzania anauchungu wa nchi.
Alisema kamati ya Bunge imeshakutana, lakini maoni waliyopendekeza juu ya mswada huo yanapaswa yapelekwe kwa Spika kwa vile suala hilo linauzito mkubwa katika kuishauri serikali.
Waziri Mkuu alisema hadi sasa bado hajapata taarifa yeyote kuhusiana na maoni ya kamati hiyo, kwa vile serikali ina nia njema ya kuridhia ili taifa liende vyema katika masuala hayo.
Aliongeza kusema kwamba, atakuwa ni mtu wa ajabu ikiwa atadharau maoni ya kamati ya Bunge watakayoyatoa dhidi ya serikali kuhusiana na mswaada huo.
“Kwa sasa siwezi kusema chochote natusubiri maoni ya kamati ya Bunge wakishawasilisha kwa Spika nitaarifiwa na tutaona wameishauri nini serikali kwa lengo la kuwa na katiba nzuri itayojenga nchi”, alieleza Waziri Mkuu Pinda.
Aidha aliwataka Watanzania wasio na hofu juu ya mswada huo kwani maoni yatayolewa na kamati ya Bunge yatazingatiwa.
Mapema Waziri Mkuu Pinda alisema hati ya dharura ya marekebisho ya mswada wa katiba iliwasilishwa Bungeni mwezi huu, baada ya kukamilika kwa mchakato wa pili wa kuundwa kwa Tume ya kamati ya katiba.
Nae Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema suala hilo limo mikononi mwake analifanyia kazi kwa kushirikiana na wataalamu wake.
Wiki iliyopita rasimu hiyo ilijadiliwa kwa jazba na kupingwa, mjadala wa Zanzibar nakala ya rasimu hiyo ilichanwa sambamba na kutiwa moto katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama cha Chadema.
Viongozi wa taasisi mbalimbali na wananchi waliipinga wakidai haina maslahi na Zanzibar, huku pia wakieleza kuwa Zanzibar haikushirikishwa kikamilifu katika uandaaji wa rasimu hiyo.
Thursday, 14 April 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment