Friday, 29 April 2011

BALOZI SEIF KUKATA UTEPE NETIBOLI A/MASHARIKI LEO

Balozi Seif kukata utepe netiboli A/Mashariki leo

Mafunzo, NIC Uganda wanawake kufungua dimba
Na Salum Vuai, Maelezo
PAZIA la mashindano ya mchezo wa netiboli kwa klabu za Afrika Mashariki, linatarajiwa kufunguliwa leo kwenye uwanja wa Gymkhana Maisara mjini hapa.
Ufunguzi huo utafanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambaye amepangwa kuwa mgeni rasmi katika siku ya kwanza ya michuano hiyo, ambapo kutashuhudiwa pambano kati ya timu ya NIC kutoka Uganda na Mafunzo ya Zanzibar kwa upande wa wanawake.
Kwa mujibu wa ratiba ya sherehe za ufunguzi iliyotolewa na Chama cha Netiboli Zanzibar (CHANEZA), timu zote zinazoshiriki mashindano ya mwaka huu zinatakiwa kuwa zimefika uwanjani ifikapo saa 8:00 mchana.
Mara baada ya mgeni rasmi kuwasili mnamo saa 10:00, wachezaji wa timu zote watapita mbele yake na wageni waalikwa kwa ajili ya maamkizi, wakiongozwa na bendi ya Jeshi la Polisi Zanzibar, na baadae wanamuziki wa bendi hiyo watapiga nyimbo za mataifa yote shiriki.
Ratiba hiyo inaonesha kuwa waamuzi wa mashindano hayo watakula kiapo cha utii na baadae kusomwa taarifa fupi ya michuano, kabla Rais wa Shirikisho la Netiboli Afrika Mashariki kutoa shukurani, kitendo kitakachofuatiwa na nasaha za mgeni rasmi.
Aidha Balozi Seif Ali Iddi atakagua timu na baadae kurusha mpira ikiwa ishara ya kuyafungua mashindano hao yanayoshirikisha timu za mchezo huo za wanawake na wanaume kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.
Mbali ya mgeni rasmi, waalikwa wengine watakaoshuhudia ufunguzi huo ni watendaji wa ngazi mbalimbali kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, wadau na wapenzi wa michezo.
Timu kadhaa miongoni mwa zile zinazoshiriki mashindano hayo, ziliwasili Zanzibar jana alasiri, huku nyengine zikitarajiwa kufika leo.
Kaimu Katibu wa CHANEZA Rahima Bakari Abdi, amesema ratiba kamili ya mashindano hayo itapangwa leo baada ya timu zote kuwasili nchini

No comments:

Post a Comment