Monday, 25 April 2011

LEO NI SIKU YA MUUNGANO

LEO NI SIKUKUU YA MUUNGANO

Muungano watimiza miaka 47 leo
• Maadhimisho kufanyika Amaan Zanzibar
• Rais Kikwete Mgeni rasmi
Na Mwandishi wetu
WANANCHI wa Tanzania, leo wanaadhimisha kutimia miaka 47 tokea kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26 mwaka 1964, uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sherehe za maadhimisho hayo yatafanyika uwanja wa Amaan Mjini Zanzibar, ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
Baada ya kupewa salamu ya heshima kwa kupigiwa mizinga 21, Rais Kikwete anatarajiwa kukaguwa vikosi vya ulinzi na usalama na baadae vikosi hivyo vitacheza gwaride la mwendo wa pole na mwendo wa haraka.
Vikosi hivyo ni pamoja na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Wanamaji, Magereza na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKT).
Miongoni mwa viongozi wa Kitaifa wataohudhuria maadhimisho hayo ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal na viongozi wengine.
Mabalozi wanaowakilisha Nchi zao hapa Tanzania nao watashiriki kwenye maadhimisho hayo, ambayo wananchi kutoka mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar watahudhuria sherehe hizo kubwa nchini.
Katika maadhimisho hayo, pia vikundi mbali mbali vya utamaduni kutoka Bara na Zanzibar vitatumbuiza, zikiwemo ngoma za asili.
Aidha wanafunzi kutoka skuli za Zanzibar na Tanzania Bara wataimba kwaya huku wakifanya onesho maalum la halaiki, maalum kwa sherehe hizo.

No comments:

Post a Comment