Tuesday, 12 April 2011

JK.; MSWADA MABADILIKO YA KATIBA BADO

JK: Mswada mabadiliko ya katiba bado


• Asema CCM panga la zamani makali yale yale
Na Rajab Mkasaba, Dodoma

MUSWADA wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bado na uliopo hivi sasa ni Mswada wa utaratibu wa namna ya kukusanya maoni na baada ya kukamilika ndio utatoa Muswada wa Katiba hiyo mpya.

Rais Kikwete aliyasema hayo wakati akifunga kikao cha siku mbili cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM) kilichomaliza juzi usiku mjini Dodoma ambacho kilipanga upya safu ya viongozi wakuu wa chama hicho.

Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema uamuzi wa viongozi hao wa CCM hivi sasa ni kwenda kutoa elimu kwa wananchi ili kuondokana na upotoshwaji unaofanywa juu ya Mswada wa Katiba hiyo.

Alisema wapo watu wanaopotosha ukweli juu ya hatua hiyo na uamuzi wa viongozi hao wa kuzunguka kueleza ukweli kwa lengo la kuwaelimisha wananchi ili kuepusha upotoshwaji unaoenezwa utasaidia kueleza ukweli.

Katika mkutano huo ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia, ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM alihudhuria, Rais Kikwete alieleza kuwa mkutano huo umefanya maamuzi makubwa na magumu lakini ulikuwa baridi na kufanyika vizuri kutokana na chama hicho kujipanga vyema.

Alisema kuwa CCM imeanza safu ya kujipanga upya hivyo umoja na mshikamano ndani ya chama hicho ndivyo vitakavyojenga na kukiimarisha Chama.

Aidha, Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa, alisema matumaini ya wanachama na viongozi wa CCM kutokana na uongozi mpya ni kukidhi haja ya kuendelea kukiimarisha chama “Panga la zamani makali yale yale”,alisisitiza Rais Kikwete.

Rais Kikwete alitoa shukurani kwa Kamati Kuu kwa uamuzi wao wa kujiuzulu kwa lengo la kukijenga upya chama na kusisitiza kuwa katika mkutano huo mambo mbali mbali wamekubaliana kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuundwa Baraza la Ushauri litakalowajumuisha wazee.

Pamoja na hayo, Rais Kikwete alieleza kuwa nguvu za chama ni wanachama na kusisitiza haja ya kukiimarisha chama ili kisionekane kuwa ni chama ambacho vitendo vya rushwa havichukizi ndani ya chama hicho.

Sambamba na hayo, Rais Kikwete alisisitiza kuwa baada ya mchakato mzima wa kupanga upya safu za viongozi nguvu kubwa hivi sasa zitaelekezwa katika kuyaimarisha Mashina na Matawi kwani huko ndiko waliko wapiga kura zaidi.

Nae, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Rajab Makamba alitoa shukurani zake kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa pamoja na Sekretarieti aliyokuwa chini yake ambayo imejiuzulu kwa mashirikiano makubwa yaliopelekea chama hicho kukipa ushindi katika uchaguzi mkuu uliopita.

Makamba alisema kuwa ameridhishwa na mchakato wote uliofanyika na kusisitiza kuwa yeye na wenziwe waliojiengua katika nyadhifa mbali mbali ndani ya chama hicho wataendelea kukiimarisha na kukiunga mkono chama hicho wakati wote.

Katibu Mkuu huyo mstaafu alisema Sekretarieti aliyokuwa akiongoza imejiuzulu kwa maslahi ya chama huku akisisitiza kuwa alikataa kujiuzulu peke yake na akieleza kuwa hivi sasa anakwenda kutayarishwa makao.

Katika uteuzi huo, Wilson Mkama amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Yusuf Makamba, ambapo Katibu Mkuu huyo mpya atasaidiwa na Naibu Katibu Mkuu Bara John Chiligati na Zanzibar, Vuai Ali Vuai.

Katibu mpya wa Itikadi na Uenezi ni Nape Nnauye, ambapo Mwingilu Mchemba amechaguliwa kuwa Katibu Idara ya Fedha na Uchumi na Mkuu wa Oganaizesheni ni Asha Abdallah Juma ambapo Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ni Januari Makamba.

Kwa upande wa Zanzibar waliochaguliwa ni Dk. Hussein Mwinyi, Dk. Maua Daftari,Samia Suluhu Hassan, Mhe. Shamsi Vuai Nahodha, Yussuf Omar Mzee, Profesa Mbarawa Mnyaa na Muhamed Seif Khatib.

Kutokana na madaraka aliyopewa Kikatiba Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Mrisho Kikwete aliteua wajumbe 10 kuingia NEC ambao ni Anna Abdallah, Peter Kisumo, Mwingilu Mchemba, Wilson Mkama, Januari Makamba, Ali Juma Shamuhuna, Dk. Emmanuel Nchimbi na Haji Omar Kheri.

No comments:

Post a Comment