Tuesday, 26 April 2011

WATOTO WADHIBITIWE WASICHEZEE MAJI MACHAFU

Watoto wadhibitiwe wasichezee maji machafu

Na Rahma Suleiman
WANANCHI wametakiwa kuwadhibiti watoto wao hasa waliochini ya umri wa miaka mitano, kutochezea maji machafu ili kuweza kuepuka maradhi ya mripuko hasa katika kipindi hiki cha mvua za masika.
Mwenyekiti wa kamati ya Mazingira na Diwani wa Viti Maalum wa Halmashauri wa wilaya ya Magharib, Halima Salum Abdallah alipokua akizungumza na muandishi wa habari hizi huko ofisini kwake.
Alisema kwa kiasi kikubwa Halmshauri imejiandaa kuiepusha jamii na maradhi ya miripuko ikiwemo kuyasafisha majaa mbali mbali kama vile Kwamchina, Kwamzungu, Mwanakwerekwe na Melinne Taveta.
Mwenyekiti huyo alitoa onyo kwa Mama lishe kuweka usafi katika maeneo yao ya biashara ili kuweza kujikinga na maradhi ya mripuko na waweze kuchemsha maji ya kunywa na wavae mavazi yenye kutambulikana.
Alifahamisha kuwa tayari wameshaandaa utaratibu wa kuvaa sare kwa mama lishe hao kinachotakiwa ni kufika katika Halmashauri ya wilaya na kufika kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira na Ustawi wa Jamii ili kuweza kupewa maelekezo ya sare hiyo.
Hata hivyo aliwataka wananchi wawe tayari kwa kulipa ada za usafi hususan katika maeneo ambayo yenye utaratibu wa kulipia ada ya utupaji wa taka na tayari wanataka kuanzisha kamati ya mazingira katika shehiya nyengine.
Pia mwenyekiti huyo aliwaomba watu wenye uwezo kuweza kujitokeza kuwajengea maslahi ya kuweza kuhifadhia taka ili kuweka mazingira safi.

No comments:

Post a Comment