Kitambi noma wapeleka mazoezi Pemba
Na Abdi Suleiman, Pemba
JAMII kisiwani Pemba, imeshauriwa kuwa na mwamko wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao na kujiepusha na maradhi mbalimbali.
Ushauri huo umetolewa na Afisa Mipango wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Pemba, Khatib Juma Mjaja, alipokuwa akizungumza na wanamichezo wa kikundi cha 'Kitambi noma' katika uwanja wa michezo Gombani.
Mjaja ambaye alikuwa akimuwakilisha Afisa Mdhamini wa wizara hiyo, alisema kuwa mazoezi ni chanzo kizuri cha kujenga afya bora kwa mwanadamu, pamoja na kuwa mazoezi ni urafiki na pia husaidia kuuweka mwili vyema na uwezo wa kujihami na matukio mbalimbali ya ghafla.
Alisema wizara yake itakuwa bega kwa bega na vikundi vinavyojihusisha na mazoezi ya viungo ili viwe endelevu, ikiamini kuwa taifa litajengwa na watu wenye afya nzuri, na kwamba mazoezi ni njia muhimu ya kutokomeza maradhi kama sukari, shindikizo la damu, kupunguza mafuta mwilini na kujijenga kisaikolojia.
Naye Katibu wa kikundi hicho Amina Talib, alisema kuwa bado mwamko wa kujiunga na vikundi vya mazoezi kisiwani Pemba ni mdogo, kwa vile watu wengi hawajui wapi pa kuanzia katika kujiunga na vikundi hivyo.
“Mtu mmoja hawezi kufanya mazoezi akiwa peke yake, bali watu wakijiunga pamoja wataweza kujiimarisha na kufanya vizuri", alisema Amina.
Alieleza kuwa lengo la ziara yao kisiwani Pemba, ni kuishajiisha jamii ili ihamasike kufanya mazoezi kwa manufaa yao na taifa kwa jumla.
Katika ziara hiyo, wanachama 50 kati ya 100 wa kikundi cha 'Kitambi noma', walitembelea wilaya tafauti za Pemba kwa muda wa siku tatu kushajiisha uundwaji wa vikundi kama hivyo.
Friday, 29 April 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment