Tuesday, 19 April 2011

JAJI MKUU ; MAJAJI,MAHAKIMU EPUKENI RUSHWA.

Jaji Mkuu: Majaji, Mahakimu epukeni rushwa

Na Nafisa madai, Maelezo

MAJAJI na mahakimu nchini wametakiwa kufanyakazi kwa kuzingatia maadili yao na kutakiwa kuachana kabisa na vitendo vyenye kuhatarisha ajira zao ikiwemo rushwa.

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud alieleza hayo kwenye hafla fupi ya kuagwa na wafanyakazi wa Idara ya Mahakama iliyofanyika hoteli ya Zanzibar Beach Resort, iliyopo nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Alisema ni wakati kwa Majaji na Mahakimu wajisafishe kwa kurejesha hadhi ya Mahakama, ili watu watambue kuwa wanapokwenda Mahakamani wanapatiwa haki na sio mtu maalum ndiye anayetoa haki kwa kupokea rushwa.

Jaji mkuu huyo alisema wanaohusika na utoaji wa haki wawe waaminifu na waondokana na vishawishi visivyokua na maslahi na kazi zao kwa kuepusha aibu, fedheha pamoja na kashfa.

Aidha alisema kuna baadhi ya watendaji hao kwao ni vigumu kutoa haki kama hajapatia chochote na anaedai haki yake jambo ambalo limekua likiharibu maadili ya kazi zao na kujishushia hadhi ya cheo alichonacho.

Alisema kazi zao zinahitaji mashirikiano na hakuna hata kiumbe kimoja katika ulimwengu huu aliekamilika hivyo ni vizuri kuuliza pale wanapokuwa na wasiwasi na kukubali kupokea ushauri ambao utaleta ufanisi katika kazi.

Alisema ufanisi utapatikana kwa wafanyakazi hao endapo watashirikiana na kupokea ushauri hali itakayojenga mazingira mazuri kwa jamii na sio kunyooshewa vidole.

“Wakati natawazwa kuwa Jaji mkuu mwaka 1989, sijawahi hata kuwa hakimu wa wilaya jambo ambalo lilinikalia vigumu kwa upande wangu maana sikujua hata pa kuanzia japo nilikua Mwanasheria Mkuu, lakini nilikubali kupokea ushauri kwa wakubwa na wadogo”, alisema Jaji Hamid.

Aidha alisema mafanikio aliyoyapata ni juhudi kubwa za pamoja na alizooneshwa na watendaji wake hivyo aliwaasa kumpa mashirikiano mazuri jaji ambae atakachukua nafasi hiyo mara tu atapoteuliwa na rais.



Akitaja sababu ya kubaki katika nafasi ya ujaji mkuu kwa muda wote hakuwahi kupokea rushwa na hakukubali hata siku mmoja kumpa haki mtu ambae hakustahili kupata haki jambo mabalo linamfanya aondoke akiwa mwenye furaha kabisa na wala hana kinyongo rohoni



Mapema akitoa shukrani zake kwa Jaji Mkuu huyo Waziri wa Katiba na Sheria Abubakar Khamis Bakary, alisema Jaji Hamid ana kila sababu ya kupongezwa kwa kufanyakazi katika mazingira magumu hasa pale anapokabiliwa na kesi ngumu za kisiasa.

Hata hivyo alisema Jaji Hamid ni mtendaji mzuri asiyekubali kurubuniwa kwa fedha wala maneno, alikuwa anahakikisha haki inatendeka kwa kila mtu, wanyonge na hata kwa wanaojiweza.

Katika risala ya wafanyakazi wa Mahakama iliyosoma na Thuwayba Haroub, alisema Jaji huyo anaondoka akiwa bado wanamuhitaji hivyo walimuomba kufungua milango wazi ili nasaha na ushauri wake uendele kupatikana.

Aidha wafanyakazi hao walimzawadiwa zawadi kadhaa akiwemo ng’ombe wa kisasa wa maziwa kwa vile Jaji huyo shughuli zake zitakuwa za kilimo na ufugaji mara atakapostaafu mwishoni mwa mwezi huu.

No comments:

Post a Comment