Tuesday 19 April 2011

Mkurugenzi wa zamani STZ afariki dunia



Mkurugenzi wa zamani STZ afariki dunia


Na Mwandishi Wetu



MTNGAZAJI mkongwe Zanzibar, Joseph Caitan Asama (79), amefariki dunia juzi mchana huko nyumbani kwake Mbweni Zanzibar.


Marehemu Asama alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa muda mrefu na alizidiwa juzi wakati akiwa katika matayarisho ya kwenda Hospitali Mnazi Mmoja kwa matibabu na hatimaye kufariki dunia.


Misa ya mazishi ya marehemu Joseph Asama itafanyika leo mchana katika Kanisa la Anglikana Mbweni nje kidogo ya Manispaa ya Zanzibar na kutarajiwa kuzikwa katika makaburi ya Mwanakwerekwe Unguja saa 9:00 Alasiri.


Viongozi mbalimbali wa juu wa serikali pamoja na wananchi wanatarajiwa kuhudhuria katika mazishi ya mtangazaji huyo mkongwe wa Sauti ya Tanzania Zanzibar.


Joseph Asama, alizaliwa Julai 12 mwaka 1932 Kisima Majongoo Unguja na ni miongoni mwa wa watangazaji wa mwanzo katika tasnia ya Utangazaji kwa wakati huo Visiwani Zanzibar.


Alianza kazi katika miaka ya mwishoni mwa hamsini katika Idara ya Habari na Utangazaji akiwa katika sehemu ya Utangazaji ya Sauti ya Unguja kabla ya kuwa Sauti ya Tanzania Zanzibar.


Ukiacha uzoefu katika utangazaji, marehemu Joseph Asama alikuwa Mkuu wa vipindi wa STZ, Mwandishi wa Habari wa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi,Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Utangazaji pamoja na kuwa Ofisa Uhusiano wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar.


Marehemu Joseph Asama, ameacha kizuka mmoja na watoto wawili.


No comments:

Post a Comment