Monday 18 April 2011

SEKRETARIETI MPYA CCM KUTAMBULISHWA ZENJI LEO

Sekretarieti mpya CCM kutambulishwa Zenji leo

Na Mwantanga Ame
MAPOKEZI makubwa yanamsubiri Katibu Mkuu mpya wa CCM, Wilson Mukama pamoja na wajumbe wengine wa kamati Kuu ya halmashauri Kuu ya Taifa watakapowasili Zanzibar leo.
Mkama aliteuliwa hivi karibuni kushika nafasi hiyo baada ya iliyokuwa sekreterieti ya Chama cha Mapinduzi iliyoongozwa na Katibu Mkuu wake Yussuf Rajab Makamba kujiuzulu.
Makamba na wenzake waliamua kuchukua hatua hiyo kabla ya kuanza kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichomalizika Makao Makuu ya Chama hicho mjini Dodoma wiki iliyopita.
Kujiuzulu kwa sekreterieti hiyo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliekiongoza kikao hicho alitangaza kuunda sekreterieti mpya kwa kumteua Mkama kushika nafasi hiyo.
Kutokana na mabadiliko hayo CCM imeamua kumtembeza kiongozi huyo katika maeneo makuu ya Chama hicho ikiwa ni hatua ya kumtambulisha rasmi ambapo tayari ameshaifanya kazi hiyo kwa wanachama wa CCM katika Mji wa Dodoma.
Mkama anatambulishwa akiwa pamoja na viongozi wengine akiwemo Naibu Katibu Mkuu mpya wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai ambapo leo wanatarajiwa kuzungumza na wananchi na wanachama wa chama hicho katika viwanja vya mwembe kisonge.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Uenezi na Itikadi ya Chama cha Mapinduzi, Katibu Mkuu huyo atawasili kwa boti katika Bandari ya Zanzibar wakati wa asubuhi na baadae kufika Ofisi Kuu ya CCM kusaini kitabu cha wageni na kuzungumza na watendaji wa Ofisi hiyo na kusalimiana na wazee.
Baada ya kufanya kazi hiyo atakutana na wanachama wa CCM katika mkutano wa hadhara utaofanyika katika eneo la Mwembe Kisonge ambapo Naibu Katibu Mkuu wa CCM bara John Chiligati atamtambulisha rasmi.
Wengine ambao ataambatana nao taarifa hiyo ilieleza ni pamoja katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM taifa Mwingulu Mchemba, Katibu wa Oganaizisheni wa CCM Taifa Asha Abdalla Juma, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Mnawiye.
Baadhi ya wanachama waliozungumza na gazeti hili wengi wao walieleza nia yao ya kujitokeza kwa wingi kuwapokea viongozi hao ambapo waliahidi kufanya hivyo kwa sherehe mbali mbali.

No comments:

Post a Comment