Zanzibar yavinjari kuimarisha magofu
Na Mwandishi wetu
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imeanza kutekeleza mkakati wake wa kuimarisha magofu ya kihistoria yaliyopo Unguja na Pemba kwa lengo la kuimarisha utalii na kusaidia wananchi kuondokana na umasikini.
Hayo yalielezwa na waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Abdilahi Jihadi Hassan, alipozungumza na waandishi wa habari baada ya ziara ya kukagua magofu kisiwani Unguja jana.
Jihadi ambae aliongozana na timu nzima ya watendaji wa Wizara hiyo, akiwemo Naibu waziri wake, Bihindi Hamad Khamis, Katibu Mkuu Dk.Ali Mwinyikai, pamoja na wakurugenzi wa taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo, amesema sekta ya magofu imetupwa kwa kipindi kirefu Zanzibar, hivyo hayakuonekana kama yana tija, lakini sasa Serikali kupitia Wizara yake itahakikisha inayaimarisha.
Waziri huyo aliwataka wananchi wanaoishi karibu na magofu hayo maeneo ya Mijini na Vijijini Unguja na Pemba, kushirikiana na serikali katika kuyaimarisha magofu hayo na kuyatumia kwa faida ya maendeleo yao na nchi yao kwa jumla.
Waziri Jihad, amesema Zanzibar inakosa fedha nyingi kutoka kwa watalii kupitia magofu, kwa vile mengi yao yamesahauliwa na kubomolewa kwa vile umakini wa kuyatunza haukuwa mkubwa.
Alisema magofu yanaweza kutoa ajira kubwa kwa wananchi wanaoishi karibu nayo, kwani mbali ya kuyatumia kwa shughuli zao za kijadi, pia yatawafungulia masoko ya bidhaa zao kwa watalii wanaofika maeneo hayo.
“Si kila mtalii anakuja Zanzibar kwa ajili ya kufuata ‘beach’ kuna wanaokuja kwa kiafya, utamaduni na wanaofuata historia ambayo inaonekana sana katika magofu, hivyo ni eneo muhimu la kulitumia kukuza utalii”, alisema Waziri Jihad.
Magofu yaliyokaguliwa jana ni pamoja na Maruhubi, Chuini, kisima cha chini kwa chini cha Mangapawani, Mnara wa kijeshi wa kupambana na meli zinazosafirisha watumwa Mangapawani na pango la watumwa Mangapwani.
Akizungumza na ujumbe huo, Sheha wa Shehia ya Mangapwani, Falabas Maridadi, alisema anaishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuyakumbuka magofu hayo kwa kuanza kuyafanyia matengenezo makubwa, kwani tayari yalishaanza kuharibika.
Sheha Maridadi alisema tayari wanakijiji wa Mangapwani, pamoja na wazee wamekubali kushirikiana na Serikali katika kuyatunza magofu hayo.
Vijana wa Mangapwani wameeleza matumaini yao ya kuinuka kiuchumi kupitia magofu hayo, kutokana na matengenezo makubwa yanayofanywa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na mradi wa MACEMP.
Mapema waziri Jihad na ujumbe wake walitembelea Chuo cha Utalii cha Zanzibar kilichoko Maruhubi, kuangalia maendeleo ya ujenzi wake na kushuhudia namna bahari inavyokula ardhi ya eneo hilo, ambapo mikakati ya kuzuia mmong’onyoko huo imepangwa na.
Tuesday, 19 April 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment