Monday, 18 April 2011

KIKWETE ATUMA RAMBIRAMBI AJALI YA ARUSHA.

Kikwete atuma rambirambi ajali ya Arusha

Na Mwandishi Maalum, Dar
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidori Shirima kutokana na ajali mbaya ya barabarani iliyotokea juzi, eneo la Makumira, Wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha na kusababisha vifo vya watu 10 na wengine wanane kujeruhiwa.
Ajali hiyo mbaya ilihusisha magari mawili ya abiria, Toyota Hiace lililokuwa likitokea Usa-River kwenda Arusha na basi la Kampuni ya Ngorika lililokuwa likitoka Arusha kwenda Dar es Salaam ambapo pia mpanda baiskeli alifariki.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na ajali hiyo mbaya ya barabarani ambayo kwa mara nyingine imepoteza maisha ya watu wetu 10 wasio na hatia,” amesema Rais Kikwete katika salamu zake hizo za rambirambi.
“Kupitia kwako wewe Mkuu wa Mkoa, ninatuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu na jamaa waliopotelewa na wapendwa wao katika ajali hii mbaya, hivyo namwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aziweke mahali pema peponi roho za Marehemu wote, Amina,” ameongeza kusema Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia amesema anamuomba Mwenyezi Mungu awajaalie wafiwa wote moyo wa uvumilivu, ujasiri na subira wakati huu wanapoomboleza vifo vya wapendwa wao na kusema kwamba yeye binafsi yupo pamoja nao katika muda wote wa maombolezo.
Kwa upande mwingine, Rais Kikwete anawaombea kwa Mwenyezi Mungu watu wote waliojeruhiwa katika ajali hiyo ili wapone haraka na kurejea katika hali zao za kawaida ili hatimaye waweze tena kuungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki zao.

No comments:

Post a Comment